MTOTO mdogo mwenye umri wa miaka mitatu mkazi wa Kijiji cha Nyamihaga
Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma amekufa baada ya kunajisiwa na baba yake
wa kambo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kigoma, Ferdinand Mtui alisema jana kwamba
wamemtia mbaroni mtuhumiwa Hamimu Saidi (27) mkazi wa kijiji hicho cha
Nyamihaga.
Akitoa maelekezo kuhusu mkasa huo, Kamanda Mtui alisema mtuhumiwa
alitekeleza dhamira yake hiyo wakati mama wa mtoto huyo ambaye alikuwa
mke wa mtuhumiwa alipokwenda kisimani kuchota maji.
Alisema baada ya mwanamke huyo kurejea nyumbani kutoka kisimani
alimshuhudia mtoto wake akilalamika sana wakati akitaka kujisaidia haja
ndogo na ndipo alipomchunguza akagundua kwamba mtoto huyo alikuwa
ameingiliwa na kujeruhiwa kwenye sehemu zake za siri.
Kamanda Mtui alisema baada ya kugundua hilo, mama huyo wa mtoto
alimchukua mtoto huyo na kumpeleka Hospitali ya Mkoa ya Maweni kwa
matibabu, ambako iligunduliwa kuwa mtoto huyo alikuwa amenajisiwa na
alikuwa amebanwa shingo wakati akifanyiwa kitendo hicho hivyo alikosa
pumzi wakati akifanyiwa unyama huo.
Kamanda huyo alisema hata hivyo mtoto huyo alifariki katika Hospitali ya
Mkoa ya Maweni alipokuwa akitibiwa na kwamba baada ya uchunguzi wa
kidaktari na uchunguzi wa Polisi, mwili wa mtoto huyo ulikabidhiwa kwa
ndugu kwa ajili ya maziko.
“Kwa sasa mtuhumiwa Hamimu Saidi anashikiliwa katika Kituo Kikuu cha
Polisi mjini Kigoma wakati upelelezi ukiendelea ili taratibu za
kumfikisha mahakamani zifanyike na kwamba anatarajia kufikishwa
mahakamani wakati wowote upelelezi huo utakapokamilika,” alieleza
Kamanda Mtui.
machupatom.blogspot.com


No comments:
Post a Comment